top of page

MPENDE JIRANI YAKO – 02 (tamati).


Mch.Madumla.

Na mchungaji G.Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Kwa ufupi,

“Mpende jirani yako kama nafsi yako” ni amri ya pili iliyo kuu. Imeandikwa;“ Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.“Marko 12:31(Ya kwanza ni mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Marko 12:30) Amri hii ilitolewa na BWANA mwenyewe tangu kipindi cha Musa,( Walawi 19:18). BWANA MUNGU aliwataka watu wake wasifanye kisasi,wala kuwa na kinyongo bali waishi maisha ya kupendana.

Mtunga Zaburi,anasema;“ Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza,Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” Zab.133:1

Kumbuka sisi tu ndugu wa BABA mmoja,MUNGU aliye hai. Na kama tu ndugu basi tunapaswa kukaa pamoja kwa umoja. Neno “pamoja kwa umoja” maana yake ni pamoja katika mwili na umoja katika roho. Hivyo basi,mtu anaweza akawa pamoja nawe lakini asiwe na umoja nawe,maana neno umoja hapo linawakilisha muambatano wa kiroho. Mfano kanisa la kwanza liliishi katika upendo pamoja kwa umoja.

Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe,wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.”Matendo 2:46-47

Tazama hapo,kanisa lilipokaa pamoja katika pendo,BWANA akalizidisha kila siku. Hata leo pia kama kweli kanisa litakaa katika pendo,basi BWANA ataonekana katika viwango vya juu. Lakini;

Kanisa la leo limepungukiwa na upendo wa ndugu,waamini hawapendani kidhati. La!kama wanapendana basi,ni ile kinafki nafki~ yaani “Upendo wa mdomoni”. Naliwaona ndugu wapendwa watatu wakiwa katikati ya mazungumzo,mmoja alikuwa akimsifia mwenzake jinsi alivyopendeza,akisema;

“shoga yangu,umependezaje! gauni limeendana na wewe alafu hilo lemba lako sasa,eeh! Yaani mule mule,umependeza sana…” gafla yule mwenye kusifiwa akaondoka. Hapo sasa! yule yule aliyekuwa akimsifia akaanza kusema“jamani, hivi huyu mwenzetu ndio kavaaje! maana mimi simuelewi elewi,yaani hasomeki!! Gauni lenyewe utafikiri kakopeshwa,bayaa….alafu hata aendani nalo,hiyo miguu sasa kama fimbo za kuchezea gofu…angelijua hata asingevaa na hilo lemba lake,yaani watu wengine sijui vipi?…”

Mwamini wa namna hii,amekosa upendo. Ni mnafiki,upendo wake ni wa kuigiza “upendo wa mdomoni” Sababu huwezi ukampenda jirani yako kisha ukamnenea mabaya kwa wengine. Ukinipenda basi usininenee mabaya.Fikiri, Je inawezekanaje mume anayempenda mke wake, amnenee mabaya kwa rafiki zake? Au mke aseme anampenda mumewe kisha amnenee mabaya kwa rafiki zake?

~Thamani ya mkristo wa kweli inapimwa katika upendo kwa jirani zake. Maana hata kama mkristo akisema anampenda BWANA MUNGU lakini akamchukia jirani yake,basi mtu huyo ni mwongo wala hampendi MUNGU. 1 Yoh.4:20

~Katika andiko letu,(Marko 12:31) tunaposoma habari za upendo tunaelewa ni nini?

Upendo maana yake ni;~Ni Roho halisi ya Mungu aliye hai. Kwa sababu Yeye Mungu ni upendo.“ Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.“1 Yoh.4:7

Upendo ~Ni roho ya kuchukuliana,kusameheana,roho ya kutohesabu mabaya ya mwenzako. Roho ya kujitoa kwa ajili ya mwenzako. Kama vile Yesu alivyojitoa kwa ajili yetu.“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;“Waefeso 5:25

Upendo haupendelei mtu bali hutenda sawa kwa wote,ukiona katika kanisa wanapendelea watu fulani hivi,basi ujue kwamba hakuna upendo wa Kristo Yesu. Mfano; kuwatenga waamini fulani kwa sababu hawana pesa,kwamba wale wenye nazo waketi hapa na wale wasionazo waketi kule mwisho kabisaa!! Yaani kana kwamba hawa wasiokuwa na uwezo mkubwa kipesa hawahitajiki. Haya ni makosa makubwa sana Yakobo 2:1-4

Wewe ambaye ni mtumishi wa Mungu,kumbuka hata kama ujaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika,ukahubiri weee kama huna upendo kazi yako ni bure.1 Wakorintho 13:1-8

Upendo~ni sehemu ya tunda la Roho,.. Wagaratia 5:22

Hivyo hatuna budi kujiuliza swali hili;

JIRANI YAKO NI NANI?

Zipo aina mbili za maana ya neno jirani,ambazo leo tunakwenda kuziangalia hapa. Maana ya kwanza;

~Jirani yako ni mtu yeyote aliye wa karibu yako kimakazi,kiofisi au popote ulipo. Jirani yako ni jirani yako tu,bila kujali ni mkristo au si mkristo,bila kujali status yake ya uchumi awe na pesa au asiwe nazo. Wala bila kujali ni mtu wa kabila yako au si wa kabila yako. Kigezo cha kumtambua yupi ni jirani yako hakipo kwa kumuangalia jinsi alivyo,bali ni vile alivyo karibu nawe. Biblia inatuagiza kumpenda jirani yetu pasipo kuangalia anasali wapi,ni mkristo au la,ni maskini au tajiri. N.K

Maana ya pili,Jirani yako ni mtu yeyote anaeweza kukusaidia pasipo kujali anaishi karibu na wewe au la, pasipo kuangalia anakujua au hakujui,pasipo kuangalia udini,ukabila au utaifa wako lakini ikiwa anaweza kukusaidia basi huyo ni jirani yako. Tuangalie biblia inasemaje kuhusu hili; Soma Luka 10:29-37.

Katika andiko hilo,watu watatu wanazungumziwa ambao ni kuhani,Mlawi na Msamaria. Katika andiko,tungemtazamia jirani yake yule aliyehumizwa angekuwa ni kuhani,au Mlawi maana hawa ndio walikuwa washika dini na ni watu wa kihuduma tofauti kabisa na Msamaria.

Tunachojifunza hapo ni kwamba kuhani na Mlawi walikuwa wakizijua sheria za kumpenda jirani kama nafsi zao lakini sheria hizo walizishika kama sheria pasipo kutenda lolote. Hali wakielekea kutimiza majukumu yao ya kidini,ndani yao masheria yapo mengi yasiyofanya kazi kwa sababu walikuwa chini ya matendo ya sheria. (Wagalatia 3:10)

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA UPENDO;

01. Pendo ni asili na tabia ya Mungu Baba,kwa sababu Yeye Mungu alitupenda sisi kwanza. “ Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.” 1 Yoh.4:19

Ikumbukwe,hapo mwanzo tulikuwa wafu kwa sababu ya makosa na maovu yetu (Waefeso 2:1). Katika hali hiyo hiyo,BWANA Mungu alitupenda;“ Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.” Waefeso 2:4. Hivyo Pendo ni asili ya MUNGU wetu.

02.Huwezi kumpenda Mungu usiyemuona ikiwa unamchukia jirani yako unayemuona.“ Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.” 1 Yoh.4:20-21

~Watu wengi leo ukiwauliza watakuambia wanampenda MUNGU hali wanawachukia jirani zao. Kumbe ni waongo sana,hata wewe yakupasa umpende kwanza jirani yako unayemuona kila siku ndiposa unaweza kusema unampenda Mungu. Ukiona mshirika aongei na mshirika mwenzake kwa sababu ya chuki,alafu mshirika huyo huyo akawa anasimama kanisani na kusema yeye ameokoka anampenda MUNGU basi huyo ni mwongo.

Ebu tujifunze kuhusu upendo wa kawaida kabisa hata kwa hawa wasiomjua Mungu watu kama wavutaji sigara,ambao utamuona mvutaji akivuta kidogo halafu anamuachia mwenzake naye avute katika sigara hiyo hiyo. Akiamini kwamba mwenzake atakata kiu ya kuvuta,lakini huku kwetu sisi wapendwa ni shida hali tunamjua Mungu japo kwa sehemu. Maana utaona mpendwa asiyekubali kushea na mwenzake hata kandambili tu. Ifike wakati sasa tubadilike!!

03.Ukikaa katika pendo,umekaa ndani ya Mungu,na Mungu ndani yako. “ Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake.” 1 Yoh.4:16

Ukitaka kujua upo ndani ya Mungu au la!basi jipime katika kipimo cha upendo. Kwa sababu ukikaa katika pendo,umekaa ndani ya Mungu,yaani ni simple kabisa kujijua upoje! 

04.Upendo una gharama.Mathayo 19:16-22

Siku zote upendo unagharama ya kutenda,maana haiwezekani kusema unampenda MUNGU pasipo kujitoa,wala haiwezekni kusema unampenda jirani yako pasipo kujitoa kwa ajili yake. Ukisoma andiko hilo hapo juu,utamuona kijana tajiri aliyezishika amri tangu utoto wake. Lakini alikuwa amepungukiwa na kitu kimoja tu,nacho ni kujitoa kwa ajili ya jirani zake maskini ambao walikuwa na uhitaji wa vitu. Bwana Yesu akamwambia aende kuuza mali zake na kuwagawia maskini kisha amfuate.

Biblia inasema “22 Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kinchoonekana kwa kijana huyu,alikuwa hawajali jirani zake maskini ingawa alikuwa ameshika sheria ya upendo kwa jirani zake.

Na ndivyo hali ilivyo hata sasa,utakuta mtu kajilimbikizia mali nyingi na wala hana msaada kwa maskini wahitaji. Wewe mwenyewe jiulize,ni mara ngapi umekwenda kuwatembelea wahitaji ? Yaani ni mara ngapi umekwenda kuwasaidia maskini wenye kuhitaji msaada,mfano wapo watu huko mahospitalini wanahitaji msaada wako. Wapo watu magerezani wenye kuhitaji msaada wako,Wapo watoto yatima na wajane wanaohitaji msaada wako. Je kama huyatimizi haya,vipi basi,unasemaje unampenda MUNGU wako? ( Mathayo 25:41-43).

Tengeneza utaratibu wa kuwatembelea watu wahitaji,kwa maana ukristo wako utakuwa na thamani kwa kufanya hivyo.

05.Mpende adui yako,muombee anayekuudhi. Mthayo 5:43-48

Ni lazima umpende adui yako na kumuombea yule anayekuudhi. Kwa sababu ipo siku moja atakuja kubadilika na kurejea kwa Mungu. Upendo wako,utamsogeza karibu na Mungu wake.

06.Msamehe jirani yako na umuachilie atoke moyoni mwako.~ Ikiwa umekwazwa na jirani yako,basi yakupasa umsamehe na usimbebe moyoni kabisa. Ukifanya hivi utaanza kumpenda taratibu hata kama alikuwa amekukosea namna gani. Kumbuka hatukuagizwa chuki,bali upendo.

HASARA ZA KUISHI NJE YA PENDO.

01. Kutawaliwa na hasira,ghadhabu na uchungu ndani ya moyo. ~ Siku zote mtu asiyependa jirani yake anakuwa ni mtu mwenye hasira,chuki na makelele. Lakini biblia inatuasa hivi;“Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.” Waefeso 4:31

02. Kutawaliwa na roho mbaya kutoka kwa shetani.

NIFANYEJE BASI?,ili niweze kuishi katika pendo nimpende jirani yangu kama nafsi yangu;

01. Omba MUNGU akusaidie kukupa roho ya kuchukuliana na jirani yako na umsamehe.“Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.” Wagaratia 6:2. Ni kweli hatufanani sote,lakini unahitaji kumuomba MUNGU akupe roho ya kuenda naye jirani yako katika udhaifu wake. Inawezekana jirani yako akawa ni mtu mkolofi,lakini jaribu kuchukuliana naye.

02. Mtendee mema unayopenda wewe kutendewa.~“Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.”Mathayo 7:12

03. Umpende sasa.

~Katika kuishi hivi kuwapenda jirani zetu,tunafaidika sisi tunaopenda. Mojawapo ya faida kubwa ipatikanayo katika pendo kwa jirani zetu ni kupata kibali katika yote tuyafanyayo. Kwa sababu kibali halisi hakiombwi ombwi bali huja kwa sababu ya kutenda mema (Mwanzo 4:7).

Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900

What’s app namba +255 746 446 446

Na. Mch.G. Madumla.

UBARIKIWE.

Yorumlar


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page