top of page

MNARA WA BABELI~Mwisho

Updated: Sep 29, 2022

Mnara wa Babeli picha na msanii wikipedia



Ikumbukwe ya kwamba, Babeli ndio mji uliokuwa wenye ustaarabu wa mambo mengi kama hali ya umoja. Katika hayo,kukazuka ibada za miungu,watu walipokusanyika pamoja hawakuwa na imani moja ya Mungu,walijawa na kiburi! Nataka ujifunze hili kwamba “ sio kweli sauti za wengi ni sauti ya Mungu” au niseme “si kweli kwamba kila haja ya wengi ipo sahihi” kwa sababu watu hawa wote walikuwa wengi waliokuwa na sauti moja lakini kule kuwa wengi hakukuwa na maana ya kwamba walinia vyema. Leo watu wengi wanajua kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,!! Sivyo hivyo bhana,inategemea ni sauti ya namna gani!!


Maana wanaweza watu wakawa ni wengi walio na sauti,lakini wakawa na nia mbaya. Sasa hapo huwezi ukasema sauti yao ni sauti ya Mungu,kama vile walivyokuwa watu wa Babeli. Ni muhimu kujua hilo,ili uwe makini na sauti za makusanyiko ya watu! Ogopa sana pale unapoona watu wamekubaliana kufanya jambo fulani nawe ukajihusisha bila kuangalia nia yao ya ndani kama ni njema machoni pa Bwana au la!


Na mara nyingi makundi au kusanyiko la watu nje ya Bwana ni ubatili! Watu wa Babeli walikusanyika pamoja na wakakubaliana kwa pamoja kujijengea mji na kilele chake kifike mbinguni;- halikuwa shauri zuri maana Mungu alitaka watawanyike wao wakati wakusanyike! Umeshawahi kujiuliza ni mara ngapi unakosea kwa sababu ya mashauri ya wengine waliokusanyika kinyume na Mungu?


Katika hayo yote,ebu leo tujifunze mambo haya,tunapojifunza habari za mnara wa Babeli;

  1. Kuchafuliwa kwa usemi.

  2. Nguvu ya umoja

  3. Mwanzo wa lugha mbalimbali.

01.Kuchafuliwa kwa usemi.


Nataka utazame usemi kama silaha kubwa ya kujenga au kubomoa kile kilichojengwa. Usemi ni ile hali ya kuelewana katika lugha. Kumbuka“ Lugha ni sauti za nasibu zenye maana” ukiona unazungumza lugha ya kwenu na mtu wa kwenu na mnaelewana ujue usemi wenu ni mmoja. Au ukiona unazungumza lugha moja ya kwenu na mtu wa kwenu lakini hamuelewani,ujue hamna semi zinazofanana ingawa lugha ni moja. Kwa lugha nyepesi ninaweza kusema usemi ni nguvu ya maelewano katika lugha. 


Adui zako wanapojipanga huwa wanazungumza lugha moja na usemi wao ni mmoja. Ili wafanikiwe ni lazima wanie mamoja wakizungumza katika semi moja. Na hicho ndicho kinachowaunganisha kutekeleza uovu wao. Babeli ilikuwa na nguvu hata watu wakatia nia ya kujenga maana walikuwa na lugha moja na usemi mmoja ( Mwanzo 11:1). Bwana Mungu alijua hilo na aliposhuka akajua silaha ile ile waliyoitumia ndio itakayowaangusha,maana Mungu alichafua semi yaani lugha yao kwamba wasielewane! 


Hata leo,ukitaka kupiga adui zako,jaribu kuchafua semi zao na hapo utakuwa umefanikiwa sana. Kwa mamlaka ile ile iliyopo ndani yako,unatamka kuwachafulia semi wale wote waliopanga mabaya juu yako watu kama wachawi kwenye vikao vyao. Ukifanya hivyo ujue hawataelewana wao kwa wao na matokeo yake utakuwa umekwisha uharibu umoja wao ( Mwanzo 11:4).


02.Nguvu ya umoja.


Ingawa nia ya watu wa waliojenga mnara wa Babeli haikuwa nzuri lakini kuna kitu kimoja cha kujifunza kutoka kwao,nacho si kingine ni “umoja”,walikuwa na umoja mkubwa sana ( Mwanzo 11:3,6). Kumbuka ule usemi “ umoja ni nguvu”. Ilikuwa ni vigumu kuwanyamazisha watu hawa sababu walikuwa na umoja,tena isingeliwezekana kwa mtu wa kawaida kuwatawanya sababu ya nguvu iliyopo katika umoja wao. Ebu jifunze kuutunza umoja wa roho,na namna ikupasavyo kutembea katika umoja.


Unajua nilikuwa ninaliangalia jambo hili kwa ukaribu sana,nikagundua kwamba hata wapumbavu katika upumbavu wao ikiwa wataungana wakawa na umoja katika upumbavu wao,ujue itakuwa ngumu sana kuufuta upumbavu wao! Ni kweli ni upumbavu,lakini kwa sababu ya umoja wao ni nani awezaye kuuvunja? Sasa fikiria watu wa Mungu wakiwa na umoja ni nguvu gani itakayowashinda? Shida iliyopo leo tumekuwa si wamoja kwa mambo ya Mungu. Maana kila mmoja anajiona kuwa ni bora kuliko wengine,tumepangalanyika. Lakini si mpango wa Mungu,maana Mungu anataka tuwe pamoja kwa umoja katika kazi yake.

“Wakasema,Haya,na tujijengee mji,…” Mwanzo 11:4 maneno haya yanaonesha makubaliano makubwa kwamba kila mmoja wao atahusika na majenzi ya mji na kinara chake. Na ndio maana Mungu akasema “…wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya” Mwanzo 11:6. Hivi unajua watu hao walikuwa hawawezekaniki kushindwa kwa jambo lolote na mtu yeyote isipokuwa Mungu tu! Mungu anasema na “tushuke huko,tuwachafulie usemi wao ” neno hilo la wingi linamaanisha Mungu mmoja katika nafsi tatu,kwa pamoja nafsi zote tatu zikashuka. Huo bado ni umoja ambao Mungu anakufundisha na wewe lazima uwe nao katika huduma,kazi,nyumbani n.k


03.Mwanzo wa kuzuka kwa lugha.


Walipokanganywa semi zao hapo ndipo lugha ilichafuliwa hata wasiweze kusikilizana,yaani sawa nakusema mmoja aliyekuwepo juu akijenga anamwambia mwenzake “naomba uniletee lami,fanya haraka” yule iliopo chini anampelekea matofali,kisha hawaelewani akisema “wewe vipi bhana,umenituma matofali na kila mtu amekusikia ukisema lete matofali,alafu unasema eti hukusema hivyo,kama vipi shuka chini nije mimi huko..” yule wa juu anapata ghadhabu,kisha anashuka huku akilalamika. Lakini huyu aliyekuwepo chini anapanda juu na kusema;


“wee fulani ebu niletee nyundo hiyo hapo chini,fanya haraka giza linaingia…” yule wa chini anainuka na kumpelekea misumari. alafu anasema“umeona…hilo ndilo tatizo lako,kumbe wewe mkolofi si umesema nikuletee misumari jamani!!! Uliza hata hawa wenzangu wamesikia hivyo hivyo” akiuliza wengine nao wanasema yakwao “ulisema akuletee chokaa” hatimaye wakawa hawasikilizani kabisa,hakuna uelewano. Wakatawanyika usoni pa nchi yote na huo ndio ukawa mwanzo wa lugha mbalimbali. 


Lazima ujifunze kufanya mambo kama ulivyoagizwa na Mungu. Ukienda kinyume ujue kuna adhabu utaipata tu,tena kamwe huwezi kufanikisha njia zako. Unajua watu hawa walipojikusanya pamoja wakajijengea jina na kutaka wasitawanyike. Fanya kama Bwana atakavyo,na utafanikiwa sana.


Kwa huduma ya maombezi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900

Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446


Mch. Gasper Madumla.


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page