top of page

MNARA WA BABELI.~01

Updated: Sep 29, 2022

Picha na wikipedia-Mnara wa babeli imechorwa na msanii Pieter Brueghel Mzee



Mnara wa babeli ni mnara mkubwa uliojengwa na kizazi cha Nuhu,Nimrodi aliyekuwa mtu hodari wa kuwinda wanyama mbele za Bwana ndie kiongozi na mmoja wa wajenzi wa mji wa mnara huu ( Mwanzo 10:9-10). Babeli ndio mji wa kwanza kujengwa kama miaka mia moja na ishirini  baada ya gharika,kumbuka Babeli ulikuwa mji wa kale sana huko Mesopotamia . Mesopotamia ilichukua eneo kubwa la kati likizunguka mito mikubwa miwili ( Tigris na Frati). Hivyo babeli kama mji wa kale na wa kwanza,ulikuwa kusini mwa Mesopotamia katika eneo linalozunguka nchi ya Iraki ya sasa.


Ndani yake Nimrodi,kulikuwa na ustaarabu wa kujikweza/kujiinua hata kupelekea hao wengine wakajiinua . Walianza kukaa pamoja walikuwa katika hali ile ile ya Nimrodi,ndipo kwa pamoja wakakubaliana kujenga mnara mkubwa “kilele chake kifike mbinguni”. Habari za mnara wa Babeli zimeandikwa kwenye kitabu cha Mwanzo 11:1-9. Watu hao wa kizazi cha Nuhu waliokaa pamoja,walikuwa na “lugha moja na usemi mmoja” ;


Moja katika ya mambo muhimu sana katika maendeleo ya mwanadamu ni matumizi ya lugha kwa maana Lugha ni chombo cha mawasiliano. Watu hawa walikuwa na usemi mmoja yaani walikuwa na uelewano wa hali ya juu sana kiasi kwamba ilikuwa ni vigumu kuwatenganisha. Siku zote watu waliokuwa na umoja huwa ni lazima wawe na lugha moja na usemi mmoja. Kumbe moja ya kielelezo cha umoja ni namna ya kuwa na “ lugha moja.” . Lakini maswali ya msingi ambayo unatakiwa kujiuliza ni kwamba, Kwa nini watu hao walijenga mnara mkubwa kama huo? Tena kwa nini walitawanywa wasimalizie kujenga? Unajifunza nini katika maisha ya sasa?

  • Makusudi ya watu kujenga mnara wa Babeli;

01. Wasitawanyike kinyume na kusudi la Mungu.( Mwanzo 11:4)


Hili ndilo kusudi mojawapo kubwa la wanadamu walianza kujenga mnara wa babeli,hawakutaka kutawanyika. Kwa sababu walikuwa wakiishi kwenye nchi tambalale na wakasema “ tujijengee mji na kinara chake kifike mbinguni” bila shaka wangetawanyika kwa sababu ya nchi walikaa ilikuwa ni tambalale. Alikuwa kusudi la Mungu watu wasitawanyike,bali Mungu alihitaji watu wakazae sana na kuijaza nchi. Ebu angalia jambo hili kwa umakini,baada ya gharika,Mungu alimbariki Nuhu na watoto wake. Baraka hiyo ilikuwa ni “baraka ya maongezeko katika uzazi “( Mwanzo 9:1).


Lakini watu walipoanza kuongezeka wakajisahau na kutaka kuendelea kukaa mahali pamoja. Kumbe;unajifunza Mungu anapendezwa na maongezeko ikiwa amesema. Hata kanisa lililojikusanya pamoja na kukosa kutawanyika kwa ajili ya kuleta maongezeko basi ujue Bwana atalitawanya tu,kusudi likaongezeke pengine na pengine na pengine. Biblia haituelezi kwamba watu wa babeli walifanya dhambi za uzinzi na uasherati bali walipishana na kusudi la Mungu kwanza.


Kusudi hili lilipelekea kutafuta jina,kwamba watu wote wakae pamoja wapate jina la kuheshimiwa hivi maana lile mnara uwe kielelezo cha kusanyiko kubwa,na hii haikuwa nzuri machoni pa Bwana. Kutawanyika kwa watu hao ndiko tunaona ongezeko likitokea kama kusudi la Mungu.


02. Kujifanyia jina


Neno hili lina maana“utambulike kwamba wewe ni nani hasa” ni hali ya kujipandisha,kutaka ujulikane,au hali ya kujiinua,kutafuta ujulikane~ leo huku kwetu Tanzania hususani Dar es salaam watoto wa mjini wanasema “kutafuta kiki”.  Sasa watu walikuwa“ wakitafuta kiki” Watu walitaka wajenge kilele cha mnara kifikie mbinguni ``ili wajifanyie jina” ( Mwanzo 11:4). Tabia ya namna hii ni kiburi na kiburi ni tabia ya shetani!!! Kulikuwa hakuna haja ya wao kutaka kujenga mpaka wafike mbinguni.!


Watu hao hawakujua kwamba wasingeliweza kufika mbinguni kwa majenzi yao waliyoanza kufanya kwa sababu hawakuwa na pesa kiasi cha kujenga mpaka kilele chake kifike mbinguni,na wala hakuna tajiri yoyote awezaye kufanya majenzi ya namna hiyo. Ukianza tu,ujue hutafika kamwe!!, Mungu afikiwi kwa majenzi kazi ya mikono ya wanadamu bali Mungu anafikiwa kwa kuoshwa kwa damu ya Yesu,katika bidii ya utakatifu.


Kumbuka hili “Kila ajikwezaye atadhiliwa“‘“ yaani kila anayejiinua atashushwa tu,hivyo ni vyema Bwana mwenyewe akuinue. Watu wa babeli walikuwa na kiburi cha kutaka kufanya kilele kifike mbinguni au mawinguni. Lakini walishushwa wote na hatimaye walishindwa kujenga mnara wao. Hivyo,babeli leo inafananishwa na tabia ya kujitengenezea jina kwa kiburi,na ndio maana hata sasa wapo watu wenye babeli zao,na hawatafanikiwa maana si tabia ya Mungu bali shetani.


Kumbuka“ Mungu hadhiakiwi”wala hakuna atakayetaka kumdhihaki Mungu na akabaki salama. Watu wa mnara walikuwa wakifanya dhiaka mbele za Mungu na hawakuachwa salama. Kiburi ni dhambi mbaya kama zilivyokuwa mbaya dhambi zote. Lakini tabia hii ndio tabia iliyowakamata watu wengi leo kiasi kwamba wamejikuta hawawezi kuendelea mbele. Hiyo ni mnara wa babeli!!!


Mimi sijui kwako kama ni mtu upendaye sana kujiinua,kujisifu sifu,jiona ona. Mtu unayetafuta jina kwamba ujulikane na watu fulani.! Kwani kuna faida gani kutafuta jina? Si afadhali ulitafute jina la Bwana Yesu kusudi uinuliwe na Bwana Yeye mwenyewe. Nimeona shida hii hata kwetu sisi tuliookoka,maana utakuta mtu “akitafuta jina ” kwa jitihada zote,akitafuta ajulikane,hivyo hana Neno bali maneno mengi ya kujiinua,kuonesha utajiri wake;

wakati mwingine hujipachika majina mengi ya ajabu ajabu mara leo utasikia akijiita nabii,kesho mtume,kesha mwalimu,


kesho yake tena mara mashine zoa zoa,mara kiboko wa wachawi,mara mzee wa Yesu Dar!!!! Hakuna tofauti kabisa na watu wale waliotafuta jina wakajipandisha wafike mbinguni lakini Bwana MUNGU akawashusha kwa anguko kubwa!!! Wewe je ukoje katika eneo hili? Chukua hatua sasa kabla ya anguko~ mshauri mwenzako mwenye tabia hii,mwambie ni kiburi hicho na abadilike au la atashushwa na MUNGU mwenyewe…


ITAENDELEA…


Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe,na msaada zaidi pamoja na maombi,nipigie sasa kwa namba hizi;+255 683 877 900


Mch. Gasper Madumla.


What’s namba ni +255 746 446 446


UBARIKIWE.

Comments


Post: MAFUNDISHO

Follow

  • Facebook
  • Twitter

©2022 by MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU. Proudly created with Wix.com

bottom of page