KUNA NENO LILILO GUMU LA KUMSHINDA BWANA? ~Mwanzo 18:14
- Mch. Gasper Madumla
- Jan 4, 2018
- 2 min read
Updated: Sep 5, 2022

Tuaenze mwaka mpya wa 2018 kwa kutafakari au kujiuliza kwamba “kuna neno lililo gumu la kumshinda BWANA? ”
Sara mkewe Ibrahimu alikuwa hazai na alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake(Mwanzo 18:11). Nao wote wawili Ibrahimu na mkewe Sara walikuwa wazee sana. Katika hali ya kawaida ilikuwa haiwezekani kwa wazee kama hawa kupata mtoto. Hii ilikuwa ni hali ya kawaida ya kibinadamu. Hata kwako inawezekana kabisa ukawa umekoma katika desturi ya wanawake ya kupata mtoto na haiwezekani kwa jinsi ya kibinadamu. Au inawezekana kabisa ukawa na jambo ambalo ukilitazama kwa jinsi ya mwili,kwa kweli haiwezekani. Lakini nataka uamini kwamba yupo Mungu awezaye kutenda hilo.
Akina Ibrahimu walikuwa na imani kubwa mbele za Mungu,lakini katika hili lilikuwa ni gumu kuamini kwamba itawezekana wao kupata mtoto.Na ndivyo ilivyo leo hii,unaweza ukawa ni mcha Mungu,mwenye imani hivi,lakini umekuwa na mipaka juu ya utendaji kazi wa Mungu hata kumuona Mungu kana kwamba hawezi baadhi ya mambo. Leo hii ebu jiulize kutoka moyoni mwako kwamba hivi kweli Mungu hawezi kulitenda hilo linalokusibu sasa? Hivi kweli jambo hilo Mungu analishindwa hata ukate tamaa?
Ukiwa unajua kwamba hakuna jambo lolote ambalo ni gumu kwa BWANA,basi huna sababu ya kuwakimbilia waganga,kuwakimbilia wanadamu kwa kutafuta misaada ya kimwili. Msaada wa kweli unapatikana kwa Bwana Mungu (Zab.46:1-2). Ikiwa Bwana aliweza kutenda kwa Ibrahimu hata akapata mtoto katika uzee wake,hivyo anaweza kukutendea na wewe sasa,ikiwa Bwana anaweza kuokoa,basi uwe na uhakika anaweza kukuokoa na wewe katika hali hiyo hiyo uliyonayo,ni kuamini tu naye atatenda katika jina la Yesu Kristo.
Mimi sijui kama unanielewa vizuri,maana hakuna linaloshindikana kwake yeye aaminiye(Marko9:23).Nami sijui kile unachopitia sasa,lakini ninachojua ni kwamba hakuna jambo lililo gumu la kumshinda BWANA. Wakati mwingine ninakosa kujua niombeje ombeje lakini pale ninapotia ufahamu na kuamua kuomba basi ninamuona Bwana akinishangaza nami ndipo ninaamini neno lake ni Amini na Kweli.
Ebu wakati huu,kwa imani uliyokuwa nayo tuombe kwa pamoja katika kile unachopitia iwe ni ugonjwa,hali ya maisha,au jambo lolote lile! Waweza kunipigia kwa simu zangu zilizopo hapo chini ili kusudi tuukabidhi mwaka huu mbele za Bwana.
Piga sasa kwa +255 683 877 900
Mchungaji Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
コメント