FAIDA YA MSAMAHA
- Mch. Gasper Madumla
- Jun 2, 2018
- 4 min read

Kumbuka Mathayo 6:14-15
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi..
Wahubiri wengi husema “ukimsamehe mtu hupaswi kukumbuka ” hivi ni kweli, ukimsamehe mtu ndio usikumbuke kabisa? Ebu chukulia mtu mmoja amekuumiza kwa hila na makusudi akakupiga na kukutoa makovu, hivi unapomsamehe kweli hutakumbuka makovu hayo yalitokea wapi? Utasahau kweli aliyekuumiza? Au chukulia umekosana na mwenzi wako wa ndoa kiasi kwamba akavunja vunja gari, akavunja vunja vyombo. Alafu ukamsamehe, je ni kweli unapoliangalia gari na vyombo vyako utasahau ni nani kavunja vunja? Jibu ni jepesi kabisa, huwezi kusahau hata moja ijapokuwa ulikwisha msamehe.
Kumbe msamaha sio suala la kutokukumbuka bali ni suala unapokumbuka unhisi nini? Ni ukweli usiopingika kwamba ikiwa umekosewa suala la kukumbuka utakumbuka tu hata kama umemsamehe lakini je unapokumbuka, ni kitu gani kinachoendelea ndani yako? Unasikia uchungu unapokumbuka au una amani tele pasipo uchungu wowote? Hayo ndio muhimu kuyajua. Mimi bhana ukinikosesha, kukumbuka nitakumbuka lakini amani na hali ya kuachiliwa itakuwepo kuonesha nimemsamehe aliyenikosa. Neno hili wengine hulitumia sivyo ndivyo;
“ Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.“ Isaya 43:25
Maana yake nini neno hilo?
andiko hili linazungumzia pande mbili, kwanza ni pande ya mkosaji na pande ya aliyekosewa. Na ndivyo msamaha ulivyo, kuna mkosaji na mkosewa. Mwanadamu amekuwa kwenye pande ya kwanza ya mkosaji na pande ya pili ni Mungu aliyekosewa. Kumbuka msamaha upo kwa sababu kuna makosa / kuumizwa n. k sasa;
Neno hilo linasema Mungu ndiye ayafutaye makosa yako kwa ajili yake mwenyewe. Hii ni sawa na kusema Mungu anakusamehe makosa yako kwa ajili yake mwenyewe, ikiwa na maana; faida ya mwenye kusamehe ipo ndani yake na wala haipo ndani ya yule anayesamehewa“ nayafuta makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe “
Mungu hasamehi kwa sababu ana shida ya kupata faida kwako, bali anatufundisha kwamba yeyote anayetaka kusamehe ni kwa faida yake mwenyewe. Ikiwa kama hujamsamehe aliyekukosea ujue atakayepata mateso siye aliyekukosea bali kwanza ni wewe uliyekosewa, maana umembeba mkosa wako.
Neno “wala sitazikumbuka dhambi zako” ni kawaida ya Mungu anaposamehe aziangalii tena dhambi ulizozitenda, ingawa anazijua zote. Vivyo hivyo nasi tunaposamehe tunatakiwa kumuona mkosa kana kwamba si mkosa tena na huku ndiko kuzisahau dhambi zetu.kumbuka ; Suala la kusamehe ni suala lisilowezekana bila Roho mtakatifu. Kwa sababu ni ngumu kusamehe, unahitaji Neema ya Bwana.
Kipimo cha kusamehewa ni kusamehe wengine
Ukipenda kusamehewa, penda kusamehe kwanza. Ndivyo neno lisemavyo kipimo kile mpiacho ndicho mtakachopimiwa. “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi.Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.Kuhusu Kufunga“ Mathayo 6:14-15
Sasa ukitaka kujua utasamehewa mangapi, jiulize umesamehe mangapi. Yaani ni kana kwamba ni biashara ya nipe nikupe! 😁😁😁. Ila iko hivi; wakati mwingine Mungu husamehe hata kuangalia kipimo chako cha kusamehe, ni huruma zake tu husamehe na kusamehe akitufundisha na sisi tusamehe bila kuchoka. Lakini kumbuka jambo moja, ukimsamehe mtu ni wewe utakaye faidika (kwa ajili yako mwenyewe).
Kuna mambo mengi yamefungwa kwa sababu ya kushindwa kumsamehe aliyekukosa. Inawezekana aliyekukoka wala hajui kama amekukosa naye anaendelea na mambo yake kama kawaida lakini wewe unaumia kwa sababu umeendelea kumshikilia. Lakini ukimsamehe mtu huyo hapo ndipo utakapouona mkono wa Bwana kwako.
Shida iko hivi, unapokwazwa, umekuwa mwepesi kukwazika na mgumu wa kuachilia. Ebu fikiria; kuna haja gani ya kuvibeba vitu vidogo vidogo visivyokuwa na mvele wala nyuma!! Ifike wakati sasa uviachilie vitu vidogo. Hivi unajua moyo wako haukuumbwa kubeba uchungu, wala kumshikilia mtu!! Ninajua kuna watu wenye digrii ya kukwaza, kuleta uchungu, nao hufurahia wakiona wamekuumiza,;lakini sikia neno la Mungu leo lisemavyo samehe hata saba mara sabini ( Mathayo 18:22). Hii ikiwa na maana samehe bila kikomo kwa yote katika hali yote.
Je unajua hata sasa unatakiwa umsamehe huyu ndugu, kwa maana baraka zako zipo hapo kwenye kusamehe. Usihesabu makosa yake, maana na wewe ukumbuke unayo yako. Bali fanya kama kwa Bwana, achilia yote na umuone kana kwamba hajakukosea. Nataka nikuambie kuna faida kubwa ukimsamehe mmoja aliyekukosa ; hivi unajua msamaha ni tabia ya Mungu maana yeye amekusamehe bure, vipi wewe unashindwaje kumsamehe ndugu huyo tena kwa kosa dogo kabisa.
Unajua unapaswa kusamehe kwa faida yako mwenyewe kwamba uhusiano wako na Mungu uzidi kuimalika. Sasa ebu fikiria kwamba mmetofautiana na mwenzako kwa muda hamuongei vizuri au hamuongei kabisa alafu kanisani mnajifanya kana kwamba mpo pamoja. Ndugu ujue, kwa mazingira haya hata sadaka yako haiwezi kupokelewa, fahamu kupokelewa kwa sadaka yako ni faida yako mwenyewe!
Mimi ninachojua ni kwamba wakati mwingine “kusamehe” ni suala gumu lakini linawezekana. Kwa sababu kama wengine tuliweza kwa msaada wa Bwana, basi na wewe leo unaweza vivyo hivyo. Mimi sijui nani alikukosea na amekukosa kwa kosa gani! Lakini kile nikijuacho ni kwamba unaweza leo kutengeneza na Mungu kwa njia ya kumsamehe na kumuachilia kabisa kwa faida yako mwenyewe. Nataka ujue kwamba Kutokusamehe ni kifungo cha uchungu, na uchungu ni mlango wa mapepo pamoja na magonjwa mbali mbali. Sasa;hakuna sababu tena ya kuendelea kuishi kwenye kifungo cha uchungu hali Umeupata ufahamu huu.
Najua mazingira mengine ni tata hata unasema sijui kama nitamsamehe kwa kosa hili?!!! Hapana leo ndio siku ya kutengeneza, ninaomba tusaidiane katika hili ili unishirikishe umekwamia wapi na tuombe pamoja na kusudi la Mungu likaonekane sasa. Waweza kunipigia kwa namba zilizopo hapa chini, wala usihofu na wala usichukue maamuzi yasiyofaa, bali nakusihi leo uchukue maamuzi mazuri ya Kiungu kwa kunipigia simu sababu Mungu anakupenda sana; piga sasa kwa-
namba hizi;+255 683 877 900
Namba ya What’sapp ni .+255 746 446 446
Mch. Gasper Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários