LANGO LA NDOTO - I
- Mch. Gasper Madumla
- Oct 5, 2018
- 4 min read
Updated: Sep 5, 2022

“ pasipo Roho mtakatifu, ndoto zinachanganya weeh acha tu!!!”
Shalom…
Kwa ufupi sana.
Ndoto ni nini?
Aina za ndoto
Tafsiri na maana zake.
01. Ndoto ni nini?
Ndoto ni njia ya kiroho ya kupata taarifa kwenye mfumo wa picha wakati mtu anapolala. Mungu hutumia mlango huu kuwasiliana na wewe mara nyingi sana,lakini shetani pia hutumia kupinga kweli. Kwa mara ya kwanza biblia inatuonesha ndoto ambapo Mungu akimtokea mfalme wa Gerari aitwaye Abimeleki (Mwanzo 20:3) ; kabla ya hapo,ndoto haikutajwa popote. Ingawa Abramu alitokewa na Mungu mara nyingi katika maono hapo mwanzo,kama katika Mwanzo 15:1 . ( Neno “ njozi ” kama lilivyotumika katika Mwanzo 15:1 halina mana ya ndoto bali lina maana ya “ maono” hivyo Bwana alimtokea Ibrahimu katika njozi,bila shaka ni Yesu ndiye aliyemtokea )
Ndoto ya Abimeleki. ( Mwanzo 20:3)
Tunaona Mungu akimwepusha Abimeleki kwamba Abimeleki asije akatenda dhambi kwa maana alimtwaa mke wa mtu,(Sara mke wa Ibrahimu) kwa makubaliano sahihi kabisa. Mungu alimwepusha mfalme huyu asije akamgusa Sara,maana itakuwa ni mbaya. Hii ndio ndoto ya kwanza kurekodiwa,na inatufundisha kwamba ndoto ni njia au mlango ambao Mungu hutumia kusema nasi,kama vile Mungu alivyosema na Abimeleki kwa njia ya ndoto.
Abimeleki alionywa vikali,naye alipoamka asubuhi alihalikisha anayatekeleza yote aliyoambiwa na Mungu katika ndoto.
Laiti kama angelipuuzia moja wapo kati ya maonyo ya Mungu basi ni dhahiri angengamia yeye na watu wake wote. Unajifunza nini hapo? Ni mara ngapi Mungu anasema nawe juu ya “ maonyo fulani ” lakini wewe hufanyii kazi na baadae unajikuta ukiangamia,alafu hapo penye maangamizi ndipo unaanza kuomba “Baba,niokoe…” sasa ulikuwa wapi muda wote usifuate tu maelekezo na maonyo uliyoambiwa. Sijui kama unanielewa!
Ebu fikiri,jinsi ambavyo Sara alivyokuwa mzuri ( tena biblia inapotaja kwamba Sara alikuwa mzuri,ujue alikuwa mzuri kweli,ule uzuri wa asili sio wa leo wa kujichubua na mkologo,na wakati mwingine mokologo wa leo unadunda,sasa hapo,wee!!! ). Kisha fikiria ambavyo makubaliano yaliyofanyika kati ya Ibrahimu na Abimeleki, lakini fikiria Abimeleki alivyofuata maonyo ya Bwana, na hatimae akashinda mtihani huo.
Ungelikuwa wewe,Je ungelifaulu mtihani huo? Au ungelisema kama wasemavyo baadhi ya walokole wa leo kwamba “ ngoja nilale naye kwanza,alafu kesho kukicha mapema kabisa nitatubu bhana….unajua,Mungu ana uhuruma,atanisamehe tu…” weeh! Mungu sio wa namna hiyo,akikuonya uwe makini kutekeleza maonyo hayo.
02. Aina za ndoto.
a) Ndoto zinazotokana na Mungu.
Mara nyingi tumesoma Mungu akiongea na watu wake kwa njia ya ndoto. Bwana anasema “Nitasema katika ndoto.” Hesabu 12:6 . Bwana alimtokea Yusufu na kumwotesha ndoto ( Mwanzo 37:5-11). Yapo maandiko mengi tu yanayoelezea jinsi ambavyo Mungu alijifunua katika ndoto na kusema na watu wake,mtazame Danieli mtu aliyependwa na Mungu, naye aliyekuwa na maono na ndoto mbali mbali.
Katika aina hii,Mungu mwenyewe amechagua namna ya kuwasiliana na watu. Hata wewe,Mungu anawasiliana nawe kwa njia ya ndoto. Wakati mwingine si lazima usikie sauti ikisema na wewe,bali Bwana anaweza kutumia lugha ya picha katika ndoto kama lengo la kuwasiliana nawe.
b)Ndoto zinazotokana na shughuli nyingi za mchana kutwa. ( Ndoto za mtu mwenyewe, mawenge wenge tu)
“ Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi;…” Mhubiri 5:3
Umeshawahi kuwa na shughuli nyingi alafu usiku ukaota jambo fulani ambalo ulikuwa ukilifanya au ulikuwa ukilifikiri sana? Ndio inakuwa hivyo. Ingawa ndoto hizi hazina maana ya kiroho,lakini unaweza ukasimama pia kwenye maombi,kwa sababu huwezi kupata hasara unapoomba kwa chochote kile.
c) Ndoto zinazotokana na shetani. ( Ayubu 7:14)
Kwa kuwa shetani ni roho,anaweza akakujia kwa njia ya ndoto na kuleta uovu wake. Wakati mwingine hujui hata kwa nini unaota unatembea na mume au mke wa mtu katika ndoto. Au wakati mwingine unaota upo kwenye mahusiano ya kimapenzi na mtu aliyekufa. Yapo mengi tu ambayo hayatokani na Mungu,shetani anaweza akakufunga katika eneo hilo.
03. Tafsiri na maana zake.
Kazi ya kutafsiri ndoto ni kazi ya Mungu ( Mwanzo 40:8b). Ni Roho mtakatifu ndiye mwenye kutasfiri mafumbo yote,kwa kuwa Yeye huchunguza yote ( 1 Wakorintho 2:10). Ukiyatambua hayo,basi huna budi kumwomba Mungu,ili akupe tasfiri ya ndoto yako. Lakini fahamu pia kazi ya kufasiri ni “ karama” yaani “ utendaji kazi wa Roho mtakatifu ” hivyo,si wote watakaoweza kukwambia maana ya ndoto yako.
Utendaji kazi wa Mungu ni wakushangaza sana,na kamwe huwezi kuuchunguza. Kwa maana tazama; mmoja apewa ndoto,mwingine apewa maarifa ya kuelekeza wapi atapata tafsiri yake,mwingine aifsiri akiongozwa na Roho mtakatifu. Sasa sikia hili; Unapoota ndoto yoyote,usikimbilie popote pale hata kwa mtumishi bali mkimbilie Mungu katika maombi wewe mwenyewe,ukiomba kwa Bwana akupe tafsiri yake kisha ndipo umwendee mtumishi wa Mungu.
Kuwa makini na vijitabu vilivyoandikwa tafsiri za ndoto!!!
Kumekuwa na desturi ya kuvitegemea vitabu vilivyoandikwa na wanadamu juu ya tafsiri za ndoto, kwamba “ukiota hivi basi ujue maana yake ni hivi…” utapotea ukivitegemea vijitabu hivyo? Kumbuka vitabu vya tafsiri sio Roho mtakatifu bali ni maarifa tu ya kawaida,tena wakati mwingine wala si maarifa ya kweli. Tegemeo lako lisiwe kwenye vitabu vya kibinadamu,bali Mungu na Neno lake ndio tegemeo lako liwe.
Huwezi kuisikia sauti ya Mungu kwa kuvitegemea vitabu hivyo!!! Matokeo yake,utakariri kila ndoto huku ukijua ikiwa hivi basi maana yake ni vile!!! Kwa sababu ndivyo ulivyoambiwa na mwandishi!!!! Ni vyema uombe kupata tafsiri yake na baada ya hapo mwone mtumishi ana kwa ana kama inawezekana…Unanielewa lakani? Haya Ubarikiwe.
Ikiwa fundisho hili limekubariki,basi ningependa kusikia kutoka kwako kwa kuniandikia msg au kunipigia kwa namba zangu zilizopo hapo juu. Pia kwa msaada zaidi pamoja na maombezi,waweza kunipigia sasa.
ITAENDELEA...
Na mch. Gasper Madumla.
What’s app ni +255 746 446 446
UBARIKIWE.
Comments