MEZA YA BWANA.
- Mch. Gasper Madumla
- Mar 5, 2017
- 3 min read

Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi;
Katika biblia kuna vifungu vinne vya maandiko matakatifu vinavyoelezea vyema kuhusu meza ya Bwana. Vifungu hivyo ni;
Mathayo 26:26-29
Marko 14:22-25
Luka 22:15-20
1 Wakorintho 11:23-25
Katika mafungu hayo ya maandiko tunaweza kujifunza mambo mengi,ikiwemo maana halisi ya “meza ya Bwana ” ,umuhimu wa meza ya Bwana katika maisha yetu ya sasa, lakini pia damu ya Yesu na umuhimu wake. ( Kwa kuwa mahali hapa ninakuandikia kwa ufupi,hivyo sitaweza kueleza hayo yote, lakini ikiwa kama una kiu ya kujifunza zaidi,basi Wasiliana nami kwa namba zangu hapo chini)
Nini maana ya meza ya Bwana?
Neno“Meza ya Bwana” huitwa pia “chakula cha Bwana,Karamu ya Bwana, sherehe ya Bwana” ni Ibada maalumu ya kula mwili na damu ya Yesu ya agano. Ukumbuke,ya kwamba kuna maagizo mawili aliyoagiza Yesu yafanyike mara kwa mara ndani ya kanisa ( agizo la kwanza ni ubatizo na pili ni kushiriki meza ya Bwana Kwa ukumbusho wake). Katika meza ya Bwana kuna vitu viwili;
Mkate – kumwakilisha mwili wa Yesu
Divai/kikombe cha baraka au kikombe cha zao la mzabibu – huwakilisha damu ya Yesu ya agano jipya
Hivyo,meza ya Bwana inaandaliwa na kuhani wa Mungu Aliye juu kwa lengo la kutimiza agizo la Bwana,pili Kwa lengo la kuachilia baraka kwa kila atakayeshiriki meza ya Bwana. – Mwanzo 14:17-19
(Meza ya Bwana ina mahusiano na “pasaka” hivyo ikiwa ni mwalimu usome kuhusu pasaka katika Kutoka 12 yote.)
Pamoja na maandiko hayo juu,biblia inataja sehemu nyingine kuhusu meza ya Bwana ingawa sehemu nyingine ni za agano la kale ambazo zilitajwa Ili kueleza meza ya Bwana itakayokuja kufanywa na Bwana Yesu mwenyewe. Angalia kama;
Kwenye hema ya kukutania ( Walawi 24:5-9)
Karamu ya pasaka ya kwanza ( Kutoka 12:13-28)
Karamu ya mwisho ya Yesu (Luka 22:14-23) Agano jipya sasa
Baada ya ufufuko wa Yesu ( Luka 24:30,41-43,Yoh.21:9-14) Agano jipya
Nani anayestahili kushiriki meza ya Bwana?
Kwa mujibu wa kitabu cha Mwanzo 14:17-19, tunamwona Ibrahimu akishiriki meza ya Bwana iliyoandaliwa na Melkizedeki kuhani wa Mungu aliye juu sana.( Melkizedeki alimwakilisha Yesu). Ibrahimu baba wa Imani anawakilisha mwamini ambaye ni safi moyoni mwake, mwamini mwenye mahusiano mema na Mungu. Hivyo,yule anayestahili kula mwili na damu ya Yesu ni yule aliyetubu dhambi zake na kuziacha,pia ni yule ambaye hana kizuizi cha dhambi
Taratibu za kushiriki
01. Kujiohoji
Paulo anatoa utaratibu wa kwanza kabisa katika kushiriki meza ya Bwana katika 1 Wakorintho 11:28 . Kwa maana aliwaona watu ambao walikuwa wakishiriki kiolela-olela yaani bila mpangilio wa kiroho. Kujiohoji kulitoa nafasi kwa kila mmoja anakuja kushiriki kujikagua moyoni. Lengo ni kutafuta nafasi ya toba kwanza kwamba Kila mshirika ajitakase kabla ya kula na kunywa damu ya Yesu ( na Kisha toba ifuate)
02. Kupatana kwanza.
1 Wakorintho 11:17-18 – anasema kukiwa na faraka ndani ya moyo wa anayeshiriki,hawezi kupata baraka badala yake atapata hasara/ laana. Hivyo,ikiwa katika kusanyiko kuna watu hawaongei kwa sababu ya kuchukiana,ni lazima wapatane Kwa upendo ndipo meza ya Bwana ifanyike. Ni jukumu pia la mchungaji kushughulikia jambo hili kabla ya meza ya Bwana kwa kutafuta suluhu.
03. Watu wangojane
Utaratibu wa kula na kunywa damu ya Yesu,unapaswa ufanyike katika hali ya utulivu kila mmoja anayeshiriki anapaswa afuate utaratibu unaotolewa na kiongozi. Ikiwa kiongozi anasema “tule mkate Sasa” basi,wote wanaoshiriki na wale mkate Kwa pamoja.
04. Maombi
Paulo anaona chakula cha Bwana si jambo dogo. Hivyo,katika kula na kunywa damu ya Yesu anaagiza maombi yafanyike kwa imani kwa sababu kuna faida ikiwa meza ya Bwana itaendeshwa katika imani ya kweli – 1 Wakorintho 11:29 Neno “ kupambanua ” ni suala la kutafakari,na kuingia katika maombi. Hivyo kiongozi atakayeongoza watu hana budi kuwaongoza watu katika maombi,
Umuhimu wa meza ya Bwana
Kuhuisha miili yetu iliyo katika hali ya kufa na kuleta tumaini jipya – Yoh.6:52-53. Isaya 53:5,-uponyaji kwa damu ya Yesu
Kuimarisha ushirika wa kanisa na WA kiroho kwa mtu mmoja mmoja -1 Wakorintho 10:16-17
Kutangaza mauti ya Kristo hata ajapo – 1 Wakorintho 11:26
Ikiwa kama umebarikiwa,nifahamishe tumtukuze Mungu pamoja. Kwa msaada zaidi na MAOMBI piga sasa kwa + 255 683 877 900
What’s app namba +255 746 446 446
Na. Mch.G. Madumla.
UBARIKIWE.
Comentários