Pamoja na kwamba baba yake Ibrahimu alikuwa ni muabudu sanamu ( Yoshua 24:2) Lakini bado Mungu alimtwaa Ibrahimu katika nyumba ya waabudu sanamu,huo ulikuwa ni mpango wa Mungu. Kumbe mpango wa Mungu hauwezi kuzuiliwa na chochote kile,ndio maana Ayubu anasema “ makusudi Yako hayawezi kuzuilika” Ayubu 42:2
“Utii wa Ibrahimu ” pale Bwana aliposema naye,lilikuwa jambo la kwanza na muhimu la kumsogeza katika baraka za Mungu hata akawa baba wa Imani kati ya mababa wengi. Inaonesha wazi ya kuwa Ibrahimu aliitambua sauti ya Bwana mapema angali alikuwa akiishi katikati ya waabudu sanamu. Kama ni hivyo,basi alikuwa ni mtu mwenye moyo wa kipekee katika nyumba ya baba yake mzee Tera. Hivyo hakuwa na mashaka kuhusu wito huo.
Kupitia hilo tu,tunaweza kujifunza kwamba unaweza ukaishi katikati ya waovu lakini wewe usiwe mwovu. Lakini pia, inawezekana kabisa kuisikia sauti/wito wa Mungu juu ya maisha yako pamoja huku ukiwa katika nyumba ya waovu. Tena, Mungu anaita mtu sio watu! Kwa maana alimwita Ibrahimu yeye kama yeye,naye akatii.
Mambo machache ya kujifunza kutoka Kwa baba wa Imani, Ibrahimu
Alimwamini Mungu,na kumwona kama baba asiyeshindwa.
Alikuwa na Utii mkubwa kwa Mungu
Alimjengea Bwana madhabahu kila alipoenda / alimwabudu Mungu mmoja wa kweli.
Kumbuka;
“utii ndio ngazi ya ukubwa na kuinuliwa” Kwa maana Ibrahimu hakufanya maajabu hata kuwa alivyo,Bali utii ndio ilikuwa maajabu yake. Hata leo,endapo kama utaitii sauti ya Bwana Kwa bidii,lazima utainuliwa na kuwa mtu Fulani wa Imani kama alivyokuwa Ibrahimu. Na tunapozungumzia kuhusu utii hatuna maana ya utii wa mambo makubwa saana kukuzidi ufahamu wako,Bali ni utii wa mambo madogo madogo ambayo Bwana amekuwa akisema nawe njia tofauti tofauti labda Kwa kinywa tu cha mchungaji wako!
Na Mch. G. Madumla